KWA NINI WATU WENGI HAWAFANIKIWI MAISHAN
Leo tunaendelea kuanzia pale tulipokuwa tumeishia, twende pamoja.
Nakumbuka siku za hivi karibuni jinsi nilivyokutana na mfanyabiashara mmoja mkubwa aliyefanikiwa sana hapa jijini Dar es Salaam. Wakati milionea huyo akifanya uamuzi wa kuwekeza kwenye biashara nyingine, watu walio karibu naye walimkatisha sana tamaa na kumwambia kuwa atapoteza.
Lakini kwa ujasiri akawajibu, ‘ninyi mnafikiri sana, lakini mimi ni mhatarishaji (risk taker)’. Baada ya kuyasikia hayo, nikatikisa kichwa kisha moyoni nikajisemea, ‘ahaa, ndiyo maana mjasiriamali huyu amefanikiwa sana maishani. Ni kwa sababu, hajali watu wanasema nini. Hakubali kukatishwa tamaa kirahisi!’
Mwandishi wa vitabu vya namna ya kusaka utajiri duniani kama vile Rich Dad Poor Dad, The Cash Flow Quadrants, Guide to Investing n.k kutoka nchini Marekani ambaye vitabu vyake vimewatoa watu wengi gizani na amehojiwa na vipindi vya televisheni vyote muhimu ulimwenguni kote kama vile Oprah, Larry King n.k, anasema kuna watu wa aina nne katika ulimwengu wa biashara.
Aina ya kwanza ni watu ambao ni lazima wawe sahihi (People who must be right). Watu hawa huwa ni vigumu sana kupokea au kukubali mawazo mapya na huwa wana mrengo mmoja tu wa kufikiri. Japo watu hawa huwa hawako tayari kuhatarisha na kufanikiwa, tunawahitaji katika nyanja nyingine maishani, mfano kama wanasheria na wahasibu.
Aina ya pili ni watu wasiotaka usumbufu (People who must be comfortable). Kwa lugha nyingine ni kwamba watu hawa wako tayari kukaa sebuleni wakinywa chai, huku nyumba inaungua. Hawako tayari kuacha starehe au kutoka katika mazingira waliyonayo ili kufanya vitu tofauti au vyenye changamoto kwa kuwa hawataki usumbufu.
Aina ya tatu ni watu ambao wanataka kupendwa (People who must be liked). Kundi hili huenda na upepo. Kwa kuwa hawapendi kuchukiwa au kubishiwa, huangalia wengine wako upande gani, kisha huungana nao.
Aina ya mwisho ni watu ambao ni lazima washinde (People who must win!). Hawa huwa kinyume na hayo makundi hapo juu. Hawa ndiyo huwa miamba. Hufanya kila wanachoweza ili kufika juu maishani.
Watapambana kwa udi na uvumba mpaka wafanikiwe.
Lakini jambo la muhimu sana ni kwamba wengi wa watu hawa huwa na ujasiri wa kukabiliana na aina tatu za kwanza hapo juu, kwani bila hivyo hao wa juu huhakikisha kuwa kundi hili linaungana nao na kuwa wapotezaji kama wao katika biashara
Je wewe msomaji, uko kundi gani? Kama ndiyo unaanza, fanya kila uwezalo kuwa na marafiki ambao wanapenda kushinda. Watafute popote pale, kwenye semina au makongamano, kwenye vikundi vya kijasiriamali au kusaidiana, kutoka kwa wateja au wagavi wako. Kwa namna yeyote ile, hakikisha unatafuta mabingwa, ili na wewe siku moja uje kuwa bingwa!
Kuna kitu fulani kizuri sana kuhusu kushinda maishani na katika biashara. Mabingwa hawawi mabingwa kwa sababu wameshinda, la hasha! Mabingwa wanashinda kwa sababu ni mabingwa kwanza.
Anza kujifua kadiri uwezavyo katika safari yako ya kuelekea kuwa bingwa ili uwe unashinda maishani. Inaanza kwanza na kubadilisha mfumo mzima wa fikra, kisha inafuatiwa na kujifunza kwa bidii kila kipengele muhimu cha biashara yao. Anza leo hujachelewa!
Mbinu ya pili ni kuamua kuwa na maktaba yako mwenyewe ya mafanikio. Hii ndiyo njia nyepesi kuliko zote kwa kuwa ni rahisi kununua vitabu kuliko kutafuta rafiki tajiri. Anza kununua japo kitabu kimoja kwa mwezi na usome kila siku japo kwa dakika 15 kama uko bize sana lakini kama una muda wa kutosha, tumia nusu saa au hata saa moja na muda mzuri ni kila asubuhi kabla hujaanza shughuli zako. Kufanya hivi kutakuweka mbele sana maishani kwa muda mfupi kuliko mtu asiyesoma chochote kila siku.
Tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment