Monday, 11 August 2014

KOCHA WA SIMBA ATIMULIWA KISA BONGO MOVIE

Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic.


UONGOZI wa Klabu ya Simba umetangaza kumfuta kazi Kocha Mkuu, Zdravko Logarusic, huku ukitaja sababu kibao.
Simba imeeleza Mcroatia huyo, amesitishiwa mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kukinoa kikosi hicho ikiwa ni siku moja mara baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Zesco ya Zambia katika mchezo uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatatu, rais wa timu hiyo, Evans Aveva, alisema kuwa maamuzi hayo wameyatoa kufuatia kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jana Jumapili asubuhi.
Aveva alisema maamuzi hayo magumu yamesababishwa na tofauti iliyopo kati ya hulka na mwenendo wa kocha huyo na desturi na utamaduni wa klabu ya Simba.
“Napenda kuwahakikishia wanachama wa Simba kuwa kutokana na dhamana kubwa waliyotupa katika kuiongoza timu yao, naomba niseme kuwa maamuzi haya yamefanyika baada ya kutafakari kwa kina.
“Ninapenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya kamati ya utendaji kumshukuru Logarusic kwa kazi kubwa katika kipindi chote alichokuwa anaifundisha Simba, hivyo tunamtakia maisha mema huko aendako.
“Tunawaomba mashabiki wa Simba kuwa watulivu katika kipindi hiki tukiendelea na mchakato wa kocha mwingine atakayekuja kuchukua nafasi yake,” alisema Aveva.

Staa wa filamu Bongo,Wema Sepetu.
Aidha, alisema utofauti huo wa kocha na klabu hiyo wamekuwa wakiuzungumza mara kadhaa na kujaribu kuwekana sawa lakini kadiri siku zilivyokuwa zikienda, hakukuwa na nafuu yoyote iliyoonekana.
Ingawa Aveva hakueleza kila kitu, lakini imeelezwa wiki mbili zilizopita uongozi wa Simba, ulimuweka kitako Loga na kumuonya kuhusiana na taarifa za kuwa na urafiki wa karibu na wasanii wa Bongo Movie, Wema Sepetu na Yvonne Cherry ‘Monalisa’.
Wema & Monalisa:
Kumekuwa na taarifa kuwa amekuwa na ukaribu na Monalisa na Wema na kuna taarifa Monalisa ambaye hivi karibuni alifiwa na mzazi mwenzake, George Tyson, alikuwa akionekana nyumbani kwa Loga eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam.
“Mona amekuwa akipika na kupakua kwa Loga, hii imesababisha wakati mwingine hata kocha ashindwe kuwahi mazoezini. President (rais), amemuita kama mara mbili kumuonya awe makini kulinda heshima ya Simba, lakini wapi,” kilieleza chanzo.
Championi Jumatatu lilimtafuta Monalisa jana ambaye alisema: “Hapana jamani hizo ni tetesi tu.”
Baada ya hapo alikata simu na alipopigiwa hakupokea na baadaye ilionekana kama alikuwa akizungumza na simu nyingine, huenda alikuwa akiwasiliana na kocha kumueleza kwamba Championi wamelitibua.
Kwa upande wa Wema, alisema: “Kweli kocha nimekuwa nikiwasiliana naye, lakini si kama mnavyofikiri. Nisingependa kuzungumzia kwa sasa.”
Msanii wa Bongo Movie,Yvonne Cherry ‘Monalisa’.
Lakini kingine kilichochangia Loga kutimuliwa ni baada ya kuwatolea lugha kali za matusi ya nguoni wachezaji wa Simba mara tu baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zesco ambayo kikosi chake kililala kwa mabao 3-0.
“Kocha kawatukana (Amri) Kiemba, (Ramadhan Singano) Messi, Abdi Banda, Uhuru (Selemani) tena bila sababu. Alilaumu kiwango chao hakikuwa kizuri lakini alitoa maneno makali sana,” kilieleza chanzo kwa mara nyingine.
Kuhusiana na uamuzi huo wa Simba, Loga alisema kinyonge kwa sauti ya huzuni: “Nisingependa kuzungumza zaidi, nasubiri kulipwa haki yangu. Mkataba wetu unasema ninatakiwa kulipwa miezi miwili kama utasitishwa. Hivyo niache kwanza nitakapomalizana nao, nitazungumza.
“Wameniambia wananiandalia tiketi niondoke keshokutwa (kesho), acha nisubiri kwanza.”
Loga aliyetua Simba baada ya kuinoa Gor Mahia ya Kenya, wiki chache zilizopita aliingia mkataba mpya wa miaka miwili kuinoa timu hiyo.

imetoka global publisher 

No comments:

Post a Comment