Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman.
Dodoma.Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman amezua
kizaazaa bungeni baada ya jana kupiga kura ya ‘hapana’ katika ibara 22
kwenye Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Akipiga kura hiyo, Othman ambaye hivi karibuni
alijiondoa katika Kamati ya Uandishi kwa kutoridhika na baadhi ya mambo,
alieleza kutokubaliana na ibara ya pili, tisa, 86, 37, 70 hadi 75 na
Sura ya 11 ambayo ina ibara ya 158, 159, 160 na 161 pamoja na Sura ya 16
yenye ibara za 243 hadi 251 na Nyongeza ya Kwanza inayozungumzia mambo
ya Muungano.
Hatua hiyo ilionekana kuwaudhi baadhi ya wajumbe
kiasi cha kumzomea, hivyo baada ya Bunge kuahirishwa alilazimika
kutolewa mlango wa nyuma wa Ukumbi wa Bunge ambao hutumiwa na Waziri
Mkuu huku akiwa amesindikizwa na wanausalama kwa kuhofia vurugu.
Wakati akisindikizwa, alikuwa ameongozana na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Waziri katika
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud na Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.
Kwanza alipelekwa kwenye chumba kimojawapo katika
jengo la Bunge ambako alikaa kwa nusu saa kabla ya kutolewa nje ya eneo
la Bunge ambako alipanda gari alilokuwamo Kificho na kuondoka.
Hatua hiyo ya Othman imekuja wakati Waziri wa
Sheria wa Zanzibar, Abubakary Khamis Bakary (CUF) akiwa hayumo bungeni
baada ya kususia vikao hivyo pamoja na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Watanzania (Ukawa).
Baadaye Othman aliliambia gazeti hili kwamba licha
ya kuwa yeye ni Mwanasheria Mkuu wa SMZ alitumia utashi wake wa
kidemokrasia kupiga kura kuzikataa ibara hizo, kutokana na kutoridhishwa
na jinsi zilivyoandikwa.
“Katika suala la Katiba, Serikali ilishatamka
kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kwamba haina msimamo.
Ndiyo maana uliona misimamo ilikuwa imeachwa kwenye vyama vya siasa,
sasa mimi siyo Mwanasheria Mkuu wa chama chochote.
“Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa
maana ya upande, maana yake ni ipi pengine unisadie… nilipiga kura kwa
kuzingatia utashi wangu na maoni yangu.”
Alisema awali, alikuwa ameamua kutopiga kura
lakini baadhi ya watu wenye busara walimshauri kutumia demokrasia yake
kuonyesha yale anayokubaliana nayo na yale asiyoyakubali… “Mtu unaweza
kuwa na msimamo fulani, lakini kwa jinsi binadamu tulivyo, siyo lazima
msimamo wako uwe sahihi, kwa hivyo na mimi niliwasikiliza watu wenye
busara nikaona ushauri wao unafaa ndiyo maana nilikwenda kupiga kura.”
Ashambuliwa bungeni
Baada ya Othman kupiga kura hiyo, Mbunge wa
Chwaka, Yahya Kassimu Issa, aliomba mwongozo wa mwenyekiti na
kumshambulia kwa hatua hiyo.
No comments:
Post a Comment