Monday 18 August 2014

FAIDA ZA NDIZI NA MTINDI KIAFYA

Leo tutazungumzia umuhimu wa ndizi, mtindi na machungwa katika miili yetu.
Kuna vyakula vya aina nyingi vinavyoupatia mwili mahitaji tofauti na leo tutaelezea faida zinazopatikana katika machungwa, mtindi na ndizi.

Sote tunaelewa kuwa ndizi mbivu ni tunda maarufu sana lakini pengine ni wachache wanaojua uwezo, faida na maajabu yaliyomo kwenye tunda hili. Ndizi ina aina tatu za kipekee za sukari zijulikanazo kama Sucrose, Fractose na Glucose na pia ina kiasi kingi cha nyuzinyuzi yaani fibre ambacho husaidia sana katika usagaji wa chakula tumboni.
Tunda hilo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nishati ya mwili, kula ndizi mbili huweza kuupatia mwili nguvu za kutosha kwa ajili ya kujitayarisha kufanya mazoezi kwa dakika 90! Pengine ndiyo sababu, ndizi zikawa tunda la kwanza linalotumiwa zaidi na wanamichezo hasa wanaokimbia mbio ndefu.
 Nishati siyo kitu pekee chenye faida kinachopatikana kwenye ndizi kwa ajili ya miili yetu, bali pia huweza kusaidia miili kuzuia magonjwa na matatizo kadhaa.
Vilevile ndizi ni chakula kinachujulikana kama tiba asilia kwa matatizo mengi ya kiafya. Ukifananisha ndizi na tufaha (apple), ndizi zina protini mara nne zaidi, sukari mara mbili, potassium mara tatu na vitamini A chuma mara tano zaidi.
Vilevile vitamini na madini nyinginezo hupatikana katika tunda hilo. Kwa kuwa na kiasi kikubwa cha chuma, ndizi husaidia uzalishwaji wa hemoglobin katika damu, hivyo kusaidia kuondoa upungufu wa damu.
Ndizi kwa kuwa na kiwango cha juu sana cha potassium na kiasi kidogo cha chumvi, hulifanya tunda hilo lifae katika kupambana na shinikizo la damu (high blood pressure).
Pia huweza kusaidia mwili katika kuimarisha uwezo wake wa kufyonza calcium, na hivyo kuifanya mifupa kuwa imara. Imeonekana kwamba ndizi husaidia ubongo na kuongeza uwezo wa kujifunza na kufahamu mambo.
Tunaweza kuwapa ndizi watoto wa shule wakati wa mitihani katika kipindi cha mapumziko, wakati wa chakula cha mchana na hata wakati wa kifungua kinywa. Ikiwa utang’atwa na mdudu, kabla ya kutumia krimu ya kuua sumu ya wadudu, jaribu kusugua sehemu ya ndani ya ganda la ndizi pale ulipong’atwa. Kufanya hivyo husaidia kupunguza maumivu, uvimbe na kuwasha. Baada ya kuzijua faida hizo za ndizi lakini tunahusiwa kuwa, tusizihifadhi ndizi kwenye jokofu.
Hizo zikiwa ni baadhi ya faida za ndizi, sasa tuziangalie pia faida za maziwa mtindi. Mtindi unaorodheshwa katika orodha ya vyakula bora kutokana na kuwa na virutubisho vingi vya aina mbalimbali ambavyo vina faida nyingi katika mwili wa binadamu.
Vikitajwa kwa uchache virutubisho hivyo ni Calcium, Phosphorus, vitamin B12, Iodine, vitamini B2, Vitamini B5, Zinc, Potassium na Molybdenum. Mbali na virutubisho hivyo, ndani ya mtindi pia kuna ‘bakteria hai’ ambao ni muhimu kiafya kwa mwili. Utafiti umeonesha kuwa, kunywa mtindi mara kwa mara, hasa kwa wazee huongeza uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa mbalimbali na kuufanya mfumo wa kinga ya mwili kuwa imara zaidi.
Mtindi umeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza ukeni.
Katika utafiti uliothibitisha suala hilo, wanawake wenye magonjwa ya kuambukiza sehemu za siri, baada ya kutumia mtindi kiasi cha paketi moja kila siku kwa muda wa miezi 6, maambukizi waliyokuwa nayo kabla yalitoweka.
Pia utafiti uliofanya na kuchapishwa katika jarida la Virutubisho la Marekani, ulionesha kuwa, unywaji wa mtindi kila siku huamsha na kuupa nguvu mfumo wa ulinzi wa mwili katika kupambana na magonjwa kadhaa ikiwemo saratani ya tumbo.
Faida nyingine inayopatikana kwenye mtindi ni kuwa na uwezo wa kupunguza mafuta mabaya mwilini au LDL cholesterol na wakati huo huo kupandisha kiwango cha mafuta mazuri mwilini yaani HDL cholesterol.
Lakini tunashauriwa kunywa mtindi usio na mafuta mengi ili kuweza kuipata faida hiyo. Mtindi pia umeonekana kusaidia kipunguza uzito na unene. Jambo la muhimu ni kuzingatia unywaji wa mtindi halisi uliotengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe na wala sio mtindi uliotengenezwa kutokana na maziwa ya unga.
Siri kubwa iliyomo kwenye mtindi asilia ni ule uchachu wake unaotokana na ‘bakteria hai’ wanaopatikana baada ya maziwa kuganda na kuchachuka ambao wana faida nyingi katika tumbo.

No comments:

Post a Comment