Saturday, 20 September 2014

KWA NINI WENGI HAWAFANIKIWI KWA BIASHARA YA DUKA?

Wengi wamekuwa na ndoto za kufungua maduka wakiamini yanaweza kuwa daraja la kuelekea kwenye mafanikio. Siyo mbaya kwani nawajua wengi tu ambao wamefanikiwa kwa kuanzisha vioski, baadaye maduka na sasa ni wafanyabiashara wakubwa.

Lakini wakati baadhi wakifanikiwa kwa njia hiyo, wapo ambao wamekuwa wakifungua maduka na baada ya muda kuyafunga huku wakiwa wameambulia hasara.
Utakuwa shahidi huko mtaani kwamba, kumekuwa na utitiri wa maduka lakini baadhi yamekuwa yakifungwa kisha wengine kufungua na baada ya muda mfupi kuyafunga.
Wapo waliochukuwa mikopo benki na kwenye taasisi mbalimbali kisha wakafungua maduka lakini wamekuwa wakiyaendesha bila mafanikio. Yaani mtaji hauongezeki badala yake kila kukicha bidhaa zinapungua na fedha haionekani.
Zipo sababu nyingi ambazo zinawafanya watu washindwe kufanikiwa kupitia biashara ya duka. Leo nitagusia chache ambazo naamini zitakuwa changamoto kwa wale walioanzisha maduka na wale wanaotarajia kufanya hivyo.
Eneo lisilo la biashara
Unapotaka kuanzisha biashara, kuchunguza eneo sahihi la kuweka kitega uchumi hicho ni muhimu sana. Huwezi kufungua duka kwenye mtaa ambao unajua kabisa wakazi wake ni watu wa kwenda kufanya shopping kwenye ‘super markets’.
Pia huwezi kufungua duka kwenye mtaa usio na watu lakini unakuta mtu anapata fremu kwa bei ndogo, anakimbilia kufungua duka bila kujiuliza sababu ya ‘ubei chee’ wa fremu.
Ni kwamba si eneo la biashara ndiyo maana gharama yake ni ndogo. Hapo ukifungua duka, andika maumivu kwani huwezi kupata wateja.
Wauzaji
Wengi hawajui tu lakini ukweli ni kwamba wauzaji hasa wale ambao wameajiriwa wamekuwa wakisababisha hasara kwa wamiliki. Unakuta kijana kaajiriwa analipwa shilingi 100,000 kwa mwezi lakini pesa ambayo anatumia bila bosi wake kujua ni mara mbili ya mshahara.
Wapo wauzaji ambao wanajua kabisa hawatadumu kwenye duka hilo, matokeo yake sasa, wanachukuwa chao mapema. Unakuta kila siku kwenye pesa ya mauzo anatoa shilingi 5,000 au zaidi, anaficha! Muuzaji huyo ni hatari sana kwa biashara yako. Ni hatari kwa kuwa, unaweza kukuta anachukuwa faida yote bila ya wewe kujua.
Kutojua mahesabu
Biashara yoyote bila kujua mahesabu huwezi kuiendesha vizuri. Hili ni tatizo walilonalo wengi. Unakuta mtu anafungua duka kwa kuwa tu amepata mkopo lakini hayuko makini kwenye mapato na matumizi. Yeye ilimradi pesa zinaingia, anachekelea, matokeo yake anabaki na sifa kwamba ana duka lakini faida ya kuwa nalo haionekani.
Mikopo
Ni kweli kukopesha hakuwezi kuepukika kwenye biashara ila ukifungua sana milango ya mkopo ni lazima utayumba. Kuna watu wengi sana ambao wamefunga maduka yako kwa kuendekeza kukopesha watu na wakati mwingine kujikopesha wenyewe.
Unakuta muuza duka anamkopesha mtu hadi pesa inakuwa kubwa kisha aliyekopa anahama mtaa baada ya kuona hawezi tena kulipa. Hiyo ni sumu ya biashara.
Wapo wengine wanaanzisha duka lakini matumizi ya nyumbani yote ni kutoka kwenye duka hilohilo bila kuwepo kwa utaratibu unaofaa. Ukifanya hivyo utashangaa duka linaisha taratibu na hatimaye unaona aibu hata ya kulifungua.
Kimsingi biashara ya duka inataka umakini. Si kila mtu anaiweza na ndiyo maana wanaofanikiwa ni wachache. Wengi wanabaki na historia tu kwamba waliwahi kufungua maduka lakini wakashindwa kuyaendesha.

No comments:

Post a Comment