Tuesday, 23 September 2014

KIFO CHA MWALIMU BAADA YA MATESO- 2

Naendelea kuwaletea mambo yaliyojiri wakati Mwalimu Nyerere alipotoka kijijini kwake Mwitongo, Butiama kwenda kutibiwa nchini Uingereza hadi kifo chake.

Agosti 26 na 27, 1999, vyombo vya habari Tanzania, kwa mara ya kwanza viliripoti wazi kwa umma kuwa hali ya Mwalimu Nyerere haikuwa nzuri, lakini wasaidizi wake walipata kigugumizi kusema ukweli, kwa kusingizia kuwa wao hawakuwa madaktari.
MWANZO HADI MWISHO
Septemba, Mosi mwaka 1999 Mwalimu, akisindikizwa na mkewe, Mama Maria na Daktari wake, Profesa David Mwakyusa, waliondoka nchini kuelekea Uingereza, ‘kuchekiwa’ afya yake, na familia ya Mwalimu waliwaambia waandishi wa habari kuwa angerudi Septemba 28, mwaka huohuo (1999).
Septemba, 22, 1999:- Siku sita kabla ya kufikia tarehe ambayo familia ya Mwalimu ilitaraji mzazi wao na kiongozi wa taifa hili angerejea nchini baada ya matibabu, Rais Benjamin Mkapa, alitangaza rasmi akizungumza na Kituo cha Televisheni cha CNN, kuwa hali ya Mwalimu kule Uingereza haikuwa nzuri.
Septemba 24, mwaka 1999:- Iliripotiwa kwamba Mwalimu alizidiwa akiwa huko Uingereza na kukimbizwa Hospitali ya Mtakatifu Thomas, ambako alilazwa akiwa hoi bin taabani.
Septemba 25, mwaka 1999:- Rais Mkapa, alimtembelea Mwalimu huko hospitalini London na kumpelekea salaamu za pole kutoka kwa Rais Jimmy Carter (Rais mstaafu wa Marekani) na siku hiyo usiku kwa sauti yenye kutetemeka na majonzi, Rais Mkapa, aliitangazia rasmi dunia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa anaumwa kansa ya damu.
Septemba 26, 1999:- Rais Thabo Mbeki (wa Afrika Kusini), alipitia London mpaka Hospitali ya Mtakatifu Thomas kumuona Mwalimu na kumpa salaamu za pole Rais Mkapa. Septemba 27, 1999:- Vyombo vya habari kwa kutumia vyanzo vyake nchini, vilibaini kuwa hali ya Mwalimu Nyerere ilikuwa mbaya mno, na aliwekewa mitambo ya kumsaidia kupumua.
Septemba 28,1999:- Mkewe Mama Maria na wanawe; Anna na Rose, walianza kumuangalia Mwalimu Nyerere kwa muda wote wa saa 24, huku Ikulu yetu (Dar es Salaam) ikitoa taarifa tata kuwa hali yake iliendelea kuwa nzuri kidogo, lakini wakati huo huo akatumwa Waziri wa Tawala za Mikoa, Kingunge Ngombale Mwiru, kwenda huko London kusimamia utoaji wa habari za ugonjwa na hali ya Mwalimu kwa ujumla.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment