Katika hali ya kushangaza, mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Ali, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar, amekamatwa na polisi baada ya kudaiwa kuunganisha visivyo halali, mitambo ambayo iliwawezesha watu kuangalia matangazo ya televisheni ya vituo mbalimbali kwa malipo rahisi.
“Hapa kuna watu kama 80 hivi wameunganishwa, wanaangalia televisheni za Azam, Zuku na nyingine kwa bei chee, lakini wanaangalia mipira, filamu na kila kitu, yaani huwezi kuamini kaka,” chanzo hicho kilinyetisha kwa OFM.
Katika kujiridhisha, kikosi kazi chini ya kamanda mkuu, kilitembelea eneo la tukio na kufanya ukaguzi wa siri, uliothibitisha kuwepo kwa huduma hiyo, lakini bila ya kuwepo kwa dekoda za vituo hivyo vya televisheni vinavyotolewa kwa malipo.
Baada ya kujiridhisha huko, OFM ilifanya mawasiliano na wahusika wa vituo hivyo, ambao nao walitembelea eneo hilo la tukio na kujionea wenyewe. Wahusika hao walikuwa ni Afisa Leseni wa DSTV na Afisa Mauzo wa Azam Tv pamoja na mtu mmoja kutoka chama cha hakimiliki cha COSOTA.
OFM iliwashauri maofisa hao kuripoti jambo hilo kituo cha polisi, ushauri ambao waliukubali na kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Oystebay ambao waliongozana na watu hao hadi Mwananyamala.
Masetelaiti alikiri kuendesha maisha kwa staili hiyo na kudai kuwa utaalamu wa kuunganisha ving’amuzi hivyo ni wake mwenyewe na amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu.
Afisa Leseni kutoka Cosota, Zephania Lyamuya alisema jamaa huyo anastahili kupelekwa Polisi kutoa maelezo kwani licha ya kutokuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo, pia amekuwa akiwanyonya waigizaji wanaostahili kulipwa kila filamu zao zinaporushwa katika televisheni za nje.
Naye Afisa Mkuu wa Mauzo kutoka kampuni ya Azam aliyejitambulisha kwa jina la Shah Seffu (pichani kulia), alisema kuwa operesheni hiyo ni moja kati ya hatua walizozipanga kumaliza tatizo la kuingilia mawasiliano ya televisheni jambo ambalo limeonekana kukua kwa kasi nchini.
Baada ya kuvikusanya vifaa hivyo vilipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay sambamba na mtuhumiwa kutoa maelezo ambapo jalada lilifunguliwa OB/RB/16106/2014, KUINGILIA MAWASILIANO YA TELEVISHENI
No comments:
Post a Comment