Nakushukuru wewe unayetuma ujumbe mfupi ukitoa maoni, kuchangia au kutaka ushauri kuhusu mambo mbalimbali, hata kama hujajibiwa elewa kwamba ujumbe wako umefika na utafanyiwa kazi.
Mada ya leo ni maalum kwa watu ambao tayari mpo kwenye uhusiano wa kimapenzi, iwe ni wapenzi wa muda mrefu, wachumba au wanandoa.DALILI ZA PENZI LILILOKUFA
Umewahi kuhisi kwamba penzi lako limefikia mwisho japo bado upo na mpenzi wako, mchumba au mumeo/mkeo? Yaani upoupo tu, zile hisia tamu za mapenzi ulizokuwa nazo wakati mnayaanza mapenzi yenu hazipo tena, hufurahii kuwa naye, hamzungumzi mkaelewana badala yake kila siku ni ugomvi na migogoro isiyoisha!
Kila unachokisema au atakachokisema hata kama ni kizuri vipi kinakuwa sawa na petroli kwenye moto, kinazidi kuchochea uhasama na chuki kati yenu. Kila mnapoanza kuzungumza, hata kama ni jambo zuri lazima muishie kutukanana, kufokeana au kupigana.
Unaishi naye nyumba moja lakini kila mmoja analala kwenye chumba chake, hata mkilala pamoja kila mmoja anageukia upande wake, hujisikii chochote juu yake, hata akiugusa mwili wako unaona kero na hutaki hata kumtazama usoni. Hujisikii hamu tena ya kuwa naye faragha, kila unachokifikiria kuhusu yeye kinakupandisha hasira na kukuudhi!
Unatamani uhusiano wenu ufikie mwisho hata sasa hivi ingawa hujui uanzie wapi… unatamani mwenza wako afe kwa ajali au apate balaa kubwa litakalowatenganisha.
Ukiona hayo yote niliyoyataja na mengine mengi yanakutokea, huo ni uthibitisho kwamba unaishi kwenye mapenzi yaliyokufa, Wazungu wanasema Dead Love. Kwa wale ambao wameishi kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu watakuwa wananielewa vizuri zaidi, kama upo kwenye penzi jipya, huwezi kuelewa vizuri.
KUACHANA NDIYO SULUHU?
Wengi wanapofikia hatua hii ya kuishi kwenye mapenzi yaliyokufa, huwa wanakosea sana kuamini kwamba njia pekee ni kuachana. Hata kama ni wanandoa na walishafanya mambo mengi pamoja ikiwa ni pamoja na kuzaa, wataishia kupeana talaka! Inasikitisha sana.Hata hivyo, hiyo siyo dawa kwani ni kuyakimbia matatizo! Utaachana na wangapi? Wataalamu wa mahusiano na mapenzi wanasema kila penzi lililokomaa, lazima lipitie kwanza kwenye hatua ya kufa, ukweli ambao ni wachache huweza kuukubali. Wahenga wanasema dhahabu ili ing’ae lazima ipitie kwanza kwenye moto.
NINI CHA KUFANYA?
1. Hatua ya kwanza, jiwekee nadhiri kutoka ndani ya moyo wako kwamba upo tayari kulifufua penzi lako lililokufa. Yawezekana wewe umeamua hivyo lakini mwenzako hayupo tayari, hilo lisikukatishe tamaa. Jiambie moyoni kwamba utafanya kila kinachowezekana kurudisha furaha, amani, hisia za mapenzi, msisimko na upendo kama ilivyokuwa wakati mnaanzisha uhusiano wenu.
2. Jipe muda wa kutafakari nini kilisababisha mwanzo mkawa na furaha na kupendana sana. Jaribu kukumbuka mambo uliyokuwa ukimfanyia mwanzo mpaka akakupenda na kuwafanya muishi kwa amani na upendo.
Anzia hapohapo, anza kufanya yale yaliyomfanya akupende mwanzo, kuwa mpole kwake, acha kumuonesha kisirani, dharau, jeuri au kujibizana naye. Badili hisia zako za ndani, badala ya kufikiria mabaya yake, fikiria yale mazuri aliyowahi kukufanyia.
3. Kubali kuwajibika. Japokuwa wengi huwa wanashindwa kwenye kipengele hiki, jibebeshe mzigo wa lawama wewe mwenyewe hata kama si kweli kwamba wewe ndiyo mwenye makosa. Jiambie mwenyewe kwamba wewe ndiyo umesababisha mfikie hapo mlipofika kwa sababu kama alikukosea, ungeweza kumsamehe kuanzia siku ya kwanza na wala msingefikia hatua hiyo.
Ukishakubali kuwajibika, utakuwa kwenye hatua nzuri ya kuzidi kumkaribia, hata ile chuki uliyokuwa nayo, utashangaa inayeyuka kama barafu iyeyukavyo juani na mapenzi yanaanza kuchanua upya moyoni mwako.
4. Muoneshe kwamba unajisikia vibaya kwa aina ya maisha mnayoishi na hata kama hajakuomba msamaha, jiambie ndani ya moyo wako kwamba umemsamehe bure na upo tayari kufungua ukurasa mwingine mpya.
Lilazimishe tabasamu kwenye uso wake, badala ya kuwa mnapishana ndani kama wanyama, anza kuwa unamtazama usoni kwa upole, hata kama yeye hatakuangalia lakini ataanza kuhisi kitu cha tofauti ambacho kitaanza kumbadilisha taratibu.
5. Msaidie kazi ndogondogo za nyumbani. Kama wewe ni mwanamke na kwa kipindi chote cha ugomvi hukuwa ukimfulia nguo, kusafisha chumba anacholala au kumuandalia chakula kizuri, jilazimishe kuyafanya hayo hata kama moyo wako unakataa. Yafanye akiwa hayupo.
Kama ni mwanaume, jitoe fahamu kwa kumsaidia kazi za nyumbani hata zile ambazo hukuwahi kuzifanya. Msaidie kuosha vyombo, kusafisha nyumba, kuwaogesha watoto (kama mlishazaa), kumfulia nguo zake au kuwaandalia watoto chakula.
Hata kama utakuwa hujamwambia neno lolote, atayaona mabadiliko na taratibu utaanza kuzigusa hisia zake kwa mara nyingine.
Muda mwingi atakuwa anajiuliza kwa nini unayafanya yote hayo kwa ajili yake na mwisho atajipa jibu kwamba kumbe bado unampenda na unamhitaji.Tukutane wiki ijayo kwa mwendeleo wa mada hii nzuri. Kwa maoni, ushauri au chochote, nicheki kwa namba hapo juu kwenye hii blog.
No comments:
Post a Comment