Friday, 26 September 2014

MBINU KUMI ZA KUFUFUA PENZI LILILOKUFA-2

Namshukuru Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo tunapokutana tena katika busati letu la mahaba, kuendelea kujadiliana kuhusu mada tuliyoianza wiki iliyopita ya mbinu za kufufua penzi lililokufa.
Kabla hatujaendelea, tujikumbushe kwa kifupi tulichojadiliana wiki iliyopita. Nilikufafanulia tafsiri ya penzi lililokufa ni ile hali ya kuishi na mpenzi wako ambaye mlipendana sana mwanzoni lakini sasa kila kitu kimebadilika.
Hampendani tena, ukuta mrefu wa chuki umejengeka kati yenu kiasi kwamba hamfurahii tena kuwa pamoja, kila mmoja anatamani uhusiano ufike mwisho aendelee na maisha yake.
Tulizichambua mbinu kadhaa zinazoweza kurudisha uhai kwenye penzi lililokufa zikiwemo kujiwekea nadhiri kutoka ndani ya moyo wako kwamba upo tayari kulifufua penzi lako lililokufa, kutafakari chanzo cha matatizo yenu na kukubali kuwajibika.
Pia tulijadili mbinu nyingine kuwa ni kumsamehe bure kabla hata hajakuomba msamaha, na kumsaidia kazi ndogondogo za nyumbani na tukamalizia kidogo kwa kuangalia mbinu ya sita ambayo ni kurejesha mawasiliano. Leo tunaendelea na mbinu nyingine zilizosalia zinazoweza kukusaidia kurejesha uhai kwenye penzi lako.
7. Rejesha mapenzi kwake
Yawezekana ikawa vigumu kwako kuanza kumpenda tena baada ya kuishi kwenye migogoro kwa kipindi kirefu lakini kama kweli unataka kufufua penzi, anza kumuonesha kwamba unampenda.
Kama unapata wakati mgumu kurudisha mapenzi, jaribu kujenga taswira kichwani mwako kwamba umekutana na mpenzi mpya na ndiyo mnaanzisha uhusiano wa mapenzi.
Kuna usemi wa Kizungu usemao: Love conquers all (Mapenzi yanashinda nguvu vitu vyote). Ukimuonesha mapenzi, migogoro, chuki na uhasama vitayeyuka vyenyewe taratibu kwa sababu penzi la kweli lina nguvu sana.
8. Uaminifu asilimia 100
Kama awali ulikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani bila sababu za msingi, badilisha ratiba zako. Kama ulikuwa unaweka password kwenye simu yako, itoe na mruhusu kushika simu yako kwa uhuru. Usiende kupokelea simu nje au pembeni, kuwa muwazi kwake kadiri uwezavyo.
Kama ulikuwa na ‘michepuko’, achana nayo kabisa na elekeza nguvu zote kwa mpenzi wako. Taratibu utaona anaanza kukuamini tena na endeleza uaminifu kadiri uwezavyo. Utaugusa moyo wake na penzi lake kwako litaanza kuchanua upya.
9. Mkumbushe maisha yenu wakati wa furaha.
Mnaweza kutazama picha zenu za harusi mkiwa pamoja au mlizopiga kipindi cha mwanzo cha uhusiano wenu. Utazirudisha kumbukumbu zake nyuma na atakumbuka matukio ya furaha zaidi kuliko maudhi.
Unaweza pia kumfanyia mambo mliyokuwa mkiyafanya pamoja kipindi mlipokuwa na furaha kama kutazama sinema nzuri pamoja, kusikiliza muziki anaoupenda au kumtoa ‘out’ kwenye mazingira mliyokuwa mkienda kipindi mapenzi yenu yalipokuwa motomoto.
10. Mfanyie mambo mazuri
Jitahidi kadiri ya uwezo wako kufanya mambo yatakayokuwa yanamfurahisha. Mnunulie zawadi, hata kama ni ndogo zitaufurahisha moyo wake. Mwambie maneno mazuri ambayo pengine ulishaacha kumwambia kwa kipindi kirefu.
Msifie kama yeye ni mrembo au hendisamu, mueleze kuwa hujawahi kupenda kama unavyompenda yeye na mchombeze kwa maneno mazuri kila mara unapokuwa karibu naye. Rudisha upendo kwa ndugu zake, marafiki zake na watu wake wa karibu.
Jitahidi kutafuta muda wa kutosha wa kukaa naye kila siku, hata kama ubize wa kazi unakuelemea, tenga muda kwa ajili ya kuwa naye, kula naye chakula cha jioni, kutoka ‘out’ pamoja na kwenda kwenye matembezi mkiwa pamoja huku muda mwingi ukijitahidi kuwa na tabasamu usoni mwako.
Uzuri wa mbinu hizi, ukizifanyia kazi kwa ukamilifu, matokeo yake yanaonekana haraka kuliko unavyotegemea. Kama huamini, anza leo na zingatia mbinu zote kisha utaona matokeo mwenyewe. Utakuwa umefanikiwa kurejesha furaha kwenye penzi lenu na atakupenda zaidi kuliko hata ilivyokuwa mwanzo. Cha msingi ni kujizuia kurudia maudhi mara kwa mara.


Imeandaliwa na Erasto J.Toga

No comments:

Post a Comment