ZIPO dalili kuwa wito wa viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wa kutaka watu kuandamana nchi nzima na migomo isiyoisha, kwa shinikizo la kutaka kusitishwa kwa vikao vya Bunge Maalum la Katiba (BMK) kunaweza kusababisha vurugu zitakazowalazimu polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuzidhibiti.
Hali hiyo inatokana na mkanganyiko uliotokea baada ya kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutamka kuwepo kwa mpango huo, ambao mara moja ulijibiwa na Jeshi la Polisi kuwa maneno hayo ni uchochezi na kwamba watadhibitiwa (kwa mabomu na virungu), huku bunge hilo likiendelea na vikao vyake bila wasiwasi.
Hata hivyo, watu wa rika mbalimbali waliohojiwa, wametaka pande zote zilizo katika mzozo huo, kutumia busara ili kufikia maafikiano yenye lengo la kudumisha amani na utulivu uliopo, vinginevyo nchi inaweza kuingia katika machafuko yatakayosababisha hasara kwa jamii nzima.
Hasara hiyo itatokana na wananchi kushindwa kwenda makazini kuhofia usalama wao wakati wa maandamano hayo na vijana wahuni kutumia mwanya huo kufanya uhalifu.
Mbowe alitoa kauli ya kuamasisha maandamano nchi nzima kushinikiza Bunge Maalum la Katiba kusitishwa katika mkutano mkuu wa Chadema uliofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar.
No comments:
Post a Comment