Je, mtoto wako ametimiza umri wa miaka 15? Je, ana tabia ya ujeuri? Mara nyingi wazazi huamini kuwa mtoto anapokuwa kwenye umri huu tabia ya ujeuri ni sehemu ya makuzi yake. Lakini hili si kweli.
Kwani siyo watoto wote wanakuwa jeuri kwa wazazi
wao. Wengi wao ni marafiki wakubwa wa mama zao. Pamoja na kuwa wakati
mwingine kugombana ni kawaida, lakini unapoona mwanao ana tabia ya
ujeuri unatakiwa kuliangalia kwa umakini suala hilo mapema.
Kwanza kabisa unatakiwa kuangalia, chanzo cha
tatizo hilo, je, jeuri hiyo ameifanya mara moja? Au amekuwa akiifanya
kila siku. Ni vizuri kama mzazi uongee na mtoto wako na kumueleza kuwa
hupendezwi na tabia yake hiyo ya ujeuri.
Pamoja na kuwa kama mzazi ungependa kuwa karibu na
mwanaye tena kwa mapenzi makubwa, lakini kuwepo kwa tabia ya ujeuri
kunaweza kuwa na umbali kati yenu.
Angalia vizuri kiini cha ujeuri wake kwa kila hatua
Ikiwa mwanao atafanya kitu, halafu unapomuuliza
akakujibu jeuri. Kabla ya kufanya chochote, angalia kwa umakini jambo
alilofanya. Je, ilikuwa ni haki yake kufanya hivyo? Je, ni nini mantiki
ya ujeuri wake huo? Ni katika kutetea kile alichofanya?
Endelea kumfuatilia, inawezekana akawa anavuka mipaka kwa tabia yake hiyo.
Kumbuka kuwa, wakati mwingine mtoto wako, huwa
hana nia ya kukuumiza, lakini inapotokea ukamkatalia kitu anachohisi
kwake ni sahihi ni jambo la kawaida hali hii hutoka hasa kwa watoto
walio kwenye umri huu.
Hivyo jaribu kuwa makini na uamuzi wako kwake. Mpe
nafasi ya kufanya kile anachoamini ni sahihi kwake alimradi tu kisiwe
na athari katika maisha yake. Kama ikitokea ukagundua tatizo ni vyema
kujadiliana naye, lakini siyo kugombana naye. Jaribu kumuelewesha
atakuelewa.
Tabia ya ujeuri kwa mtoto inatakiwa kuchukuliwa
hatua mapema sana kabla haijakomaa, vinginevyo inaweza kuota mizizi na
kuwa kero hata kwa jamii itakayomzunguka mtoto wako.
Mpe nafasi ya kuwa na wenzake
Katika kipindi hiki mtoto huwa na tabia ya kujiona
hana hatia lakini ukweli ni kwamba kipindi hiki mtoto huwa katika
hatari ya kujifunza kila kitu kilicho mbele yake. Kwani huwa katika hali
ya kutaka kujaribu vitu vingi zaidi kuliko awali.
Inawezekana mkawa mmegombana na mtoto wako. Ikiwa atataka kutoka
kwenda kwa rafiki zake, mpe nafasi ya kufanya hivyo, kwani huko watampa
moyo na pia watampa matumaini mapya.
Kitendo cha kumgombeza na kumfungia ndani,
kitachangia kwa kiasi kikubwa kumfanya ajione hana maana na hivyo
kupandikiza jeuri ndani yake.
Kwa kupata sapoti kutoka kwa rafiki zake,
itasaidia kumfanya apunguze hasira na wakati mwingine kurudisha maisha
yake katika hali ya kawaida.
Mawasiliano ni muhimu kati yako na mwanao
Watoto wengine kuiga tabia ya ujeuri kutoka kwa rafiki zao na kwenda kuyafanya majumbani kwao.
Ni vyema kuikomesha haraka tabia hiyo kabla
haijaota mizizi. Jaribu kuitafutia suluhisho bila kukosana naye.
Mazungumzo ni muhimu zaidi katika kumrekebisha mwanao. Hakikisha huna
hasira wakati unapofanya mazungumzo haya.
Muulize kwa nini anadhani kukufanyia ujeuri ndiyo
njia sahihi ya kudai haki yake. Ikiwa utampa maneno ya busara kuhusiana
na jinsi mtoto anavyotakiwa kumjibu mzazi wake, ni wazi kuwa atakuelewa.
Mawasiliano ni nguzo muhimu katika malezi.
Jitahidi uelewe ni kwa nini hasa anafanya jeuri. Na ni nini hasa anachokiwaza kichwani kwake.
Unapokuwa umeelewa hayo, unatakiwa kumfahamisha kuwa hata akiwa na hasira kiasi gani, hapaswi kukufanyia jeuri.
Mwelekeze mwanao kuwa kuna tofauti kubwa baina ya
familia yenu na familia ya rafiki zake. Unajua wakati mwingine marafiki
nao wanaweza kuwa chanzo cha ujeuri kwa mtoto wako ingawaje si kwa
asilimia kubwa.
Hakikisha mwanao anaelewa tofauti hiyo na kuona
umuhimu wa kutochanganya mambo na kuhamisha tabia ya rafiki yake
nyumbani kwako. Mfahamishe, kila nyumba ina muongozo wake hivyo kama
mtoto anatakiwa kufuata kile unachotaka wewe kama mzazi wake na si
vinginevyo.
IMEANDALIWA NA ERASTO TOGA
IMEANDALIWA NA ERASTO TOGA
No comments:
Post a Comment