TUNAENDELEA kuchambua hatua sita za tatizo la Ukimwi (HIV) kwenye mwili wa binadamu, endelea.
Ndani kabisa ya kiini au capsid kuna aina tatu tofauti za vimeng’enyo au enzymes ambavyo ni muhimu mno kwa ajili ya uzalianaji wa HIV. Vimeng’enyo hivyo hujulikana kama reverse transcriptase, integrase na protease. Pamoja na vimeng’enyo hivyo, capsid pia ina nyuzi mbili za vinasaba vya RNA ambavyo husaidia kurithisha tabia za vinasaba za HIV kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Ikilinganishwa na makundi mengine ya viumbe hai yenye vinasaba vingi, HIV ina vinasaba vya aina tisa tu.
Vinasaba vitatu viitwavyo gag, pol na env hufanya kazi ya kubeba taarifa inayohitajika kuunda protein muhimu kwa ajili ya virusi wapya watakaozaliwa.
Vinasaba sita vilivyobaki vinavyojulikana kama tat, rev, nef, vif, vpr na vpu hufanya kazi ya kubeba taarifa ya kuthibiti uzalishaji wa protini inayohusika na kuthibiti uwezo wa HIV kushambulia seli mpya za binadamu, kuzaa virusi wapya au kusababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu.
CD ni kifupi cha maneno ya Kingereza ya cluster of differentiation. Hii ni aina mojawapo ya kiasili kilichoundwa kwa protini na mafuta (yaani glycoprotein) ambacho kinapatikana juu ya uso wa seli nyeupe za damu zijulikanazo kama T helper cells, regulatory T cells, monocytes, macrophages, na dendritic cells ambazo kazi yake kubwa ni kupambana na maradhi mbalimbali. Zimepewa jina la CD4 kuonesha kuwa ni aina ya nne katika kundi la viasili vya CD.
Vilipewa jina hilo mwaka 1984 ingawa viligunduliwa mwishoni mwa miaka ya sabini.
Kazi kubwa za CD4 ni kusaidia baadhi ya chembe nyeupe za damu kupambana na wadudu waenezao maradhi mbambali katika mwili wa binadamu.
Kwa kutumia sehemu yake ambayo ipo ndani ya seli za T cell, CD4 husaidia kukuza na kupitisha taarifa kutoka kwenye vipokeo vilivyopo kwenye T Cell.
Taarifa hii huzitaadharisha chembe nyeupe za damu kujiandaa kupambana na vijidudu vilivyovamia mwili kwa kutumia njia mbalimbali.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment