Danny Welbeck.
BAADA ya David Beckham,
sasa ni zamu ya Paul Scholes. Nyota wote wawili hawa hawaelewi ni kwa
nini Manchester United imeamua kumuuza Danny Welbeck kwenda Arsenal.
Welbeck aliyekulia United tangu akiwa na umri wa
miaka sita alikamilisha uhamisho wa kwenda Arsenal siku ya mwisho ya
kufungwa kwa dirisha la uhamisho Jumatatu usiku, huku akionekana kama
mchezaji anayeweza kuziba pengo la Olivier Giroud aliyeumia.
Kuondoka kwa staa huyo wa England mwenye umri wa
miaka 23 kumechukuliwa na wengi kama kupisha njia kwa staa wa kimataifa
wa Colombia, Radamel Falcao aliyechukuliwa kwa mkopo kutoka Monaco
mchana wa siku hiyo.
Hata hivyo, licha ya ujio wa Falcao, Scholes
anaamini kwamba bado Welbeck angeendelea kuwa mchezaji muhimu wa siku za
usoni na kuondoka kwake ni faida kubwa kwa Arsenal ambayo imemnasa.
“Kwa ukweli nimehuzunika sana kumwona Welbeck
akiondoka. Hisia zangu ni kwamba kama angefanikiwa kubaki katika dirisha
hili angeweza kuwa sehemu ya Manchester United kwa miaka michache
ijayo,” alisema Scholes.
“Inaonyesha ni kwa kiasi gani Danny anavyoonwa kwa
sasa jinsi klabu kubwa kama Arsenal ilivyoamua kumsaini. Atakuwa
mchezaji mzuri kwa Arsene Wenger. Danny hawezi kufunga mabao 20 au 25
kwa msimu, lakini anaweza kuipatia Arsenal mabao 10 hadi 15.”
Pamoja na kuondoka kwa Welbeck, Scholes bado ana hamu ya kuona jinsi safu ya ushambuliaji ya United yenye Wayne Rooney, Robin van Persie na Falcao itakavyozinyanyasa safu nyingi za ulinzi katika Ligi Kuu England.
“Nilimtazama Radamel Falcao akiwa Porto, Atletico Madrid
na Monaco niliona jinsi alivyokuwa na mienendo ya hatari na rekodi za
ufungaji. Kwa United, uhamisho wake wa mkopo unaleta ushindani mkubwa,”
aliongeza Scholes.
“Hata hivyo, sioni namna ambavyo Louis van Gaal
anaweza kuwapanga wote watatu, Rooney, Robin van Persie na Falcao kwa
pamoja. Inabidi achague wawili kutoka kwa watatu na ni wawili gani hao?
Ni vigumu kusema.
“Sidhani kama wanaweza kutwaa ubingwa wa ligi
lakini kuingia Ligi ya Mabingwa Ulaya inawezekana. Ni juu ya Van Gaal
kuitengeneza timu.”
No comments:
Post a Comment